Dar es Salaam.Taasisi 1,200 duniani zitampa aliyekuwa mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema, Edward Lowassa Tuzo ya Amani kutokana na utulivu aliouonyesha
kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza na Mwananchi kutoka Bukavu, DR Congo, mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii, Mchungaji William Mwamalanga
alisema Lowassa amechaguliwa jana mjini Bukavu na wajumbe 1,400 wa mkutano
huo.
Mwamalanga alisema wajumbe wanaohudhuria kongamano la amani wanatoka mataifa
ya Ulaya, Marekani, Asia na Afrika kwa kuwashindanisha wanasiasa 1,000 ili
kumpata Kiongozi Bora wa Amani mwaka 2015, ambaye anajali na kuangalia maslahi
ya jamii badala ya madaraka.
Hatua ya kumpatia tuzo Lowassa ni baada ya kuelezwa kuwa amedumisha amani
hiyo hata baada ya kushindwa uchaguzi Mkuu wa Rais Oktoba 25.
Katika uchaguzi uliopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)ilimtangaza Dk John
Magufuli kuwa mshindi kwa kupata kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia 58.46 wakati
Lowassa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Mchungaji Mwamalanga alisema katika kongamano hilo, wajumbe walijadili hali
ya amani duniani na mchango wa wanasiasa katika kulinda amani hiyo.
Alisema kuwa wanasiasa barani Afrika wamekuwa vyanzo vya migogoro na mauaji
ya raia wakati wa uchaguzi, kama ilivyo nchini Burundi. Hata hivyo, alisema kuwa
wajumbe walipongeza ushindi wa Dk Magufuli, lakini wakasema umetiwa dosari na
hali ya kisiasa Zanzibar baada ya matokeo kufutwa.
Alisema wajumbe wa kongamano hilo linaloshirikisha maaskofu, masheikh na
vijana kutoka madhehebu mbalimbali ya dini barani Afrika, wamemuhimiza Rais
Magufuli kumaliza utata wa uchaguzi wa Zanzibar.
Baada ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Chadema, Lowassa alitangaza
kuwa angefanya kampeni kistaarabu na kwa amani na baada ya matokeo aliwatuliza
wafuasi wa chama hicho, akisema “hakuna anayeweza kuizuia bahati ya mtu” kwa
hiyo kama amepangiwa kuwa rais, atakuwa.
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne,
aliongeza upinzani kwenye uchaguzi wa mwaka huu baada ya kuihama CCM na kujiunga
na Chadema iliyoukuwa na nguvu ya vyama vingine vitatu vya NLD, CUF na
NCCR-Mageuzi.
Kama alivyoahidi, Lowassa hakutumia mikutano yake ya kampeni kushambulia mabo
binafsi ya wagombea wengine, bali muda mfupi kuomba kura.
No comments:
Post a Comment