Translate

Sunday, August 30, 2015

MWAKYEMBE AIBUA UPYA SAKATA LA RICHIMOND!

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza sakata la upewaji zabuni ya mabilioni ya kufua umeme kwa kampuni ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe ameibua upya suala hilo.

Mwakyembe aliyasema hayo mbele ya maelfu waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli katika viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya, jana. Akizungumzia madai ya kwa nini baadhi ya wahusika hawakupelekwa mahakamani kama kuna ushahidi, mhadhiri huyo wa sheria alisema kosa la jinai, halina ukomo na wakati wowote linaweza kufunguliwa mashitaka, huku akiapa kuwa anaweza kumfungulia mtu mashitaka hata kesho. Alionya viongozi na makada wa Chadema na vyama vinavyowaunga mkono katika umoja wa Ukawa wanaozindua kampeni zao leo jijini Dar es Salaam, kwamba wasithubutu kujibu hoja zake.

Dk Mwakyembe alisema ikilazimika kusema ukweli, ataweka hadharani uchafu wote uliofanyika, ambao alisema bungeni kuwa asingeuanika na kuifanya Richmond hoja ya kila siku mpaka Watanzania waelewe kilichofanyika. “Tunao ushahidi. Hawa walitakiwa kuwa jela badala ya kuimba nyimbo za ajabu,” alisema Dk Mwakyembe katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja nchi nzima na kuongeza kuwa Dk Magufuli akiingia madarakani, anakwenda kuanzisha Mahakama ya Ufisadi.

Alisema yeye na wenzake walipewa kazi ya Bunge kuchunguza ilikuwaje viongozi waandamizi wakaamua kuipa kampuni hewa zabuni ya mabilioni ya fedha, ambayo imesababisha mpaka leo kuna shida ya umeme nchini. Dk Mwakyembe alikumbusha kuwa walikwenda mpaka Marekani kuchunguza uwepo wa kampuni hiyo iliyodaiwa kutoka katika nchi hiyo, na kukutana na kampuni ya kuchapisha kadi za harusi.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, baada ya kubaini ubadhirifu huo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alishinikizwa kujiuzulu na kumaliza suala hilo na hivyo hatua ya kiongozi huyo kutaka kwenda Ikulu, wazalendo hawawezi kuikubali. “Hatutaruhusu watumie demokrasia kuingia Ikulu na hiyo ndiyo shida ya kuazima wagombea,” alisema Dk Mwakyembe akimaanisha kuwa chama cha Chadema, kimeazima mgombea bila kumfahamu. Dk Mwakyembe alisema suala hilo lilishafungwa bungeni, lakini anashangaa kusikia linarejeshwa kinyemela.

No comments:

Post a Comment