Translate

Tuesday, September 15, 2015

RAISI KIKWETE AMWAMBIA Mh TUNDU LISSU AMTAJE MMILIKI WA RICHMOND

Rais Jakaya Kikwete amesema anashangazwa na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kumtaka amtaje mhusika wa Richmond wakati mwenye Richmond yupo na anatembea naye mikoani.

Kikwete aliyasema hayo jana wakati akiwaaga wananchi wa Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika na kumtaka Lissu amtaje mwenye Richmond.

“Endapo Tundu Lissu atashindwa kumtaja mwenye Richmond, nitatoka hadharani na kumtaja mwenyewe,” alisema Kikwete.

Kabla ya mkutano huo, Rais Kikwete alifungua jengo la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (NSSF) ambalo limejengwa kwa Sh7 bilioni.

Akifungua jengo hilo, aliwaomba wawekezaji na mifuko ya kijamii kuiga mfano wa NSSF kwa kuwekeza katika sekta ya majengo kwa kuwa yanapendezesha mji.



Kadhalika, Rais Kikwete alizindua jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na nyumba 36 za bei nafuu zilizopo katika eneo la Mlole, Kigoma Mjini.

Richmond

Suala la Richmond imekuwa moja ya ajenda za CCM katika kampeni za urais hasa baada ya Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyejiuzulu wadhifa huyo kwa kashfa hiyo kuhamia upinzani.

Kila sehemu ambako mgombea urais wa CCM anakwenda, suala hilo limekuwa likiibuliwa, huku Lowassa akisema yeye hakuhusika, bali alijiuzulu kuiokoa Serikali isianguke kwa kuwa ulikuwa uamuzi wa wakubwa.

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amekuwa akienda mbali zaidi akisema akichaguliwa ataanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia mafisadi wanaosababisha umaskini nchini.

Bashe ataka mahakama ya mafisadi mapema

Wakati Magufuli akiahidi mahakama hiyo, mgombea ubunge Jimbo la Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alimtaka mgombea huyo jana kuiwahisha mapema iwezekanavyo akiingia Ikulu la sivyo atakuwa akihoji bungeni kila mara.

Bashe alisema akipatiwa ridhaa na wakazi wa jimbo hilo kuingia bungeni hatakuwa mbunge wa “ndiyo mzee” badala yake atakuwa akiisumbua Serikali mara kwa mara likiwamo suala la kudhibiti ufisadi nchini.

“Umesema utafungua mahakama ya mafisadi na majizi... nikuhakikishie waziri wako wa sheria utakayemteua ajue atakutana na mtu anaitwa Bashe, kila akiingia bungeni nitakuwa namuuliza kila mara upo wapi muswada wa sheria ya kuanzisha mahakama maalumu ya mafisadi na majizi,” alisema Bashe na kushangiliwa.

“Ni lazima tufike mahali Taifa hili tuache kuwa watu wa porojo....Taifa hili siyo maskini kuna wezi wapo bandarini. Najua saa hizi wanatafuta biashara nyingine.”

Mgombea huyo alisema wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais, kulikuwa na makundi ndani ya chama akiwamo na yeye lakini baada ya kumpata, Dk Magufuli tofauti zimekwisha.

Bashe alikuwa miongoni mwa vinara wa kumuunga mkono mgombea wa urais wa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa wakati akiomba ridhaa ya kuteuliwa na CCM kabla ya kuhamia upinzani.

Hata hivyo, jana alisema hataihama CCM kwa kuwa yeye na chama hicho hawakukutana barabarani na kwamba ni muumini wa mabadiliko ndani ya chama hicho.

Huku akigusia tuhuma zilizowahi kuvuma za yeye kuwaambia wananchi wamchague yeye halafu urais wampigie Lowassa, Bashe alisema wanaNzega watampigia kura Dk Magufuli asilimia zote na zikipungua hazitazidi asilimia tano.

Bulembo amvaa Sumaye

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo amemvaa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na kumtaka aache kuchukua mshahara na kurudisha walinzi wanaomlinda iwapo ataendelea kukitusi chama hicho kwamba hakijafanya chochote tangu uhuru.

Akiwahutubia wakazi wa Nzega jana, Bulembo alisema maisha yote ya kiongozi huyo na familia yake yametengenezwa na CCM lakini anashangaa kuona sasa anasimama kwenye majukwaa na kuwaeleza wananchi kuwa CCM haijafanya kitu.

“...Analipwa asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu aliyepo madarakani, Mizengo Pinda. Mpaka leo bado ana ulinzi na anahudumiwa na Serikali hii. Kwa kupitia jukwaa hili la Nzega hebu Sumaye aache mshahara huo, arudishe walinzi awe raia kama sisi,” alisema Bulembo.

Aliendelea kurusha vijembe kwa kiongozi huyo akidai kuwa alinyang’anya ardhi ya wana ushirika wa Mvomero mkoani Morogoro baada ya kutetereka.

Magufuli na michango ya shule

Dk Magufuli jana aliendelea na kampeni zake mkoani Tabora na kuahidi kuwa akiingia madarakani atafuta michango yote shuleni inayosababisha baadhi ya wazazi washindwe kuwapeleka watoto shule.

Alisema anatambua kuwa baada ya sera yake ya elimu bure kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne kuanza kutekelezwa iwapo atachaguliwa, kuna baadhi watu wataanzisha michango isiyo na maana na kwamba atawashughulikia.

“Kuna mambo ya kuwaambia wazazi peleka dawati, peleka dawati na hata kama mtoto wa kwanza akishamaliza shule, ukimpeleka mwingine lile dawati hulikuti. Ninafahamu haya yote nitayashughulikia lakini pia, hakuna sababu shule kukosa madawati au viti wakati ipo karibu na miti, mbao zipo, haya yote tutaangalia tukizingatia masilahi ya walimu wetu,” alisema Dk Magufuli.

Akiwa Bukene wilayani Nzega, Dk Magufuli aliwatahadharisha makandarasi wazembe walioshindwa kukamilisha miradi yao kwa wakati akiwataka kufanya hivyo kabla ya Oktoba 25 kwa kuwa yeye ni kiboko yao.

Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment