Translate

Wednesday, May 25, 2016

POLISI ZANZIBAR YAWATAHADHALISHA VIONGOZI WA CUF VISIWANI HUMO

Jeshi la Polisi Zanzibar, limesema kuwa vitendo vya kihalifu vya uvunjifu wa amani vinavyotokea kisiwani Pemba vinachochewa na viongozi wakuu wa chama cha Wananchi CUF.


Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, naibu mkurugenzi wa upelelezi na Makosa ya jinai wa Jeshi hilo, Salum Msangi alisema kuwa viongozi wakuu wa CUF wamekuwa wakiwatuma wafuasi wao kufanya vitendo vya hujuma kisiwani Pemba kwa madai kuwa serikali iliyopo madarakani sio halali.
 
Alisema kuwa jeshi la polisi linataarifa za uhakikia kuhusu viongozi wa CUF wakiwapongeza wafuasi wao na kuwapa zawadi ya fedha kwa kuweza kufanya vitendo vya hujuma kisiwani humo ikiwemo uchomaji moto wa majengo mbalimbali na kuhujumu mikarafuu na mazao mbalimbali.
 
“Tunao ushahidi viongozi wa CUF wamewakusanya wafuasi wao na wanawapa pongezi wale ambao wameza kufanikiwa kufanya vitendo vya hujuma dhidi ya wananchi”alisema.
 
Alisema kuwa jeshi hilo halitamvumilia mtu yoyote atakaehusika kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na wala halitakua na muhali katika kuchukua hatua za kisheria bila ya kujali cheo cha mtu.
 
Aidha alisema kuwa jeshi hilo linawashikilia watu zaidi ya 20 kisiwani Pemba ambapo wanahusishwa na vitendo vya uvunjifu wa amani na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
 
Akizungumzia kuhusu ripoti ya Chama cha wananchi CUF waliyoitoa juzi ya kulipeleka Jeshi hilo mahakama ya kihalifu ya kimataifa (ICC),alisema jeshi hilo haliogopi kupelekwa huko na kusema kuwa taarifa zilizomo katika ripoti hiyo zinazohusu jeshi la polisi ni za uongo.
 
“Kama ICC tutaanza kuwapeleka wao viongozi wakuu wa CUF ambao wao ndio wachochezi wakubwa wa uvunjifu wa amani ya nchi na taarifa zao zote tunazo”alisema Msangi.
 
Hata hivyo alisema jeshi la polisi linaendelea kuwaita watu mbalimbali na kuwahoji akiwemo Katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho.
 
Jeshi hilo liliwapa tahadhari viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kuwashawishi wafuasi wao kufanya vitendo vya hujuma wakati wao wametulia majumbani mwao.

No comments:

Post a Comment