Translate

Sunday, June 25, 2017

SERIKALI KUZIBANA KAMPUNI ZA MAFUTA NA GESI

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezitaka kampuni zilizowekeza katika sekta ya mafuta na gesi nchini, kuhakikisha zinanunua huduma na bidhaa zinazopatikana nchini ili kwenda na mahitaji yanayoendana na Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015, inayosisitiza huduma hizo kununuliwa kutoka kwa Watanzania.
Samia aliyasema hayo wakati akizundua Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) jijini Dar es Salaam, ambako pia alipongeza uanzishwaji wa jumuiya hiyo kwa kuwa una lengo sawa na Serikali ya Awamu ya Tano.

“Na pale ambapo huduma na bidhaa hazipatikani nchini, basi makampuni hayo yanapaswa kununua kutoka kwenye makampuni ya ndani yenye wabia nje ya nchi,” alisema Makamu wa Rais .
Alifafanua kuwa sheria hiyo imezingatia maslahi ya wananchi, ikitaka hisa za kampuni za ndani kutopungua asilimia 25 na kwamba kwa kununua bidhaa na huduma kutoka ndani ya nchi, Watanzania wengi walioko vijijini watanufaika.
Alisema kutokana na jumuiya hiyo, fursa mbalimbali zitapatikana ikiwemo kusaidia katika kubainisha kampuni na taasisi wenyeji wenye ujuzi na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali zinazohitajika katika miradi mikubwa.
“Wapo wawekezaji ambao wamekuwa wakisema kampuni za ndani hazikidhi vigezo vyao, ni muhimu mkazisaidia kampuni za ndani ili ziweze kukidhi vigezo katika utoaji wa huduma,” alisema na aliutaka umoja huo kuhakikisha unazisaidia kampuni za ndani ili kukidhi vigezo na hivyo wawekezaji kukosa sababu.
Alisema pia kupitia jumuiya hiyo itasaidia kuhamasisha matumizi ya nguvu kazi na bidhaa zilizopo nchini na kupunguza kuagizwa kutoka nje na pia itasaidia mapokezi ya ufundi, ujuzi na teknolojia.
Aliongeza kuwa kama wakijipanga vizuri hata wawekezaji watawapa ushirikiano mkubwa kwa kuwa wameamua kutatua tatizo linalowahusu na wao na serikali itakuwa bega kwa began a umoja huo ili kufikia malengo.
Awali, Mwanzilishi wa jumuiya hiyo, Abdulsamad Abdulrahim alisema lengo lao ni kuhakikisha wanashirikiana na serikali ili kutimiza lengo la serikali la kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao ikiwemo mafuta na gesi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Umoja huo, Balozi Ombeni Sefue alisema kupitia umoja huo lengo la Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli la Watanzania kunufaika na rasilimali zao litatekelezeka.
“Kazi inayoweza kufanywa na Mtanzania apewe Mtanzania isitoshe kusema watu wenu hawana uwezo, kama kuna mapungufu tujue yako wapi na tyarekebishe haraka,” alisema Balozi Sefue.

No comments:

Post a Comment