Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe
Hai. Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe amesema maisha ya Watanzania leo ni magumu kuliko wakati wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alikosoa kauli za Serikali kuwa uchumi unakuwa akisema uchumi huo unakuwa katika mifuko ya kikundi cha watu wachache.
Mbali na suala, Mbowe ambaye ni na Mbunge wa Hai aliishutumu Serikali ya CCM kwa matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha za walipa kodi ambazo zitatumika katika chaguzi katika kata ambazo Madiwani walijiuzulu.
Akihutubia wakazi wa kijiji cha Shirinjoro katika jimbo lake jana, Mbowe alisema hali ya maisha ya Watanzania ni mbaya kuliko kipindi cha Kikwete na kwamba kipato cha mwananchi kimeshuka.
“Serikali inasema uchumi unakuwa, tukiwauliza ni viashiria gani vinawafanya muone uchumi unakuwa wanakwambia tumenunua ndege tano na tunajenga reli ya kisasa,”alisema Mbowe na kuongeza;
“Kama uchumi unakua basi unakua katika mifuko ya kikundi cha watu wachache na sio Watanzania tunaowafahamu ambao maisha yamekuwa magumu kuliko wakati wa Kikwete.”
Mbowe alitumia fursa hiyo kuwahoji wananchi ni kipindi gani maisha ni magumu kati ya utawala wa Kikwete (2005-2015) na wa Rais John Magufuli na kujibiwa kuwa ni wakati wa Magufuli.
Kwa mujibu wa Mbowe, wakati Serikali ikijitapa kukuza uchumi, lakini hali ya maisha kwa Mtanzania imekuwa ngumu kutokana na kushuka kwa kipato na kupanda kwa gharama za maisha.
Mbowe alitolewa mfano kuwa wakati uchaguzi ukifanyika mwaka 2015, kilo moja ya sukari ilikuwa Sh1,600 lakini sasa imepanda na kufikia karibu Sh3,000 vivyo hivyo kwa bidhaa nyingine muhimu.
Mbali na suala hilo, lakini alizungumzia hatua ya madiwani wake watatu kujiuzulu na kujiunga na CCM, akisema uchaguzi wa marudio utatafuna kodi za walipa kodi zaidi ya Sh750 milioni.
“Mwaka 2015 katika kata yenu mlimchagua Mzee Kimath (Ernest) lakini ni jambo la aibu CCM kupitia mkuu wa wilaya ya Hai (Gelasius Byakanwa) wanarubuni madiwani wetu,”alisema Mbowe.
“Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa sababu gharama za kurudia uchaguzi hapa kata ya Mnadani pekeee ni Sh250 milioni. Hizi zingeweza kweda kujenga mashule na zahanati,”alisisitiza.
“Serikali inaona kuliko kuwe na diwani wa upinzani bora turudie uchaguzi kwa gharama ya mamilioni. Nataka niwaambie nitalala hapa Shirinjoro tukirudia uchaguzi na haiendi popote,”alisema.
Mbowe alitumia mkutano huo kuwaeleza wananchi hao kuwa ataendelea kupigania haki za Watanzania hata kama kwa kufanya hivyo atapelekwa gerezani akisema magereza yametengenezewa wanadamu.
“Tunaifanya kazi hii kwa maumivu makubwa ya kifamilia. Tunaifanya kazi hii kwa maumivu makubwa ya kibiashara na kisiasa. Wanadhani wanatunyong’onyeza lakini wanatuimarisha,”alisema.
“Kazi ya mageuzi ni ya muda mrefu na sio kazi ya masikhara . Ni kazi ya wito inayohitaji uvumilivu. Kama unaroho ndogo huwezi kuwa mpinzani Tanzania. Mimi nimejitoa kwa ajili ya Watanzania”.
“Hawatazuia nguvu ya mageuzi ndio maana hata Rais ana hofu, hajiamini kuwa amekuwa Rais. Hakuna mikutano ya kisiasa tukutane 2020 wakati yeye kila siku anapiga siasa,”alisema Mbowe.
“Sitakaa kimya na siku nikikaa kimya nitakuwa kaburini. Magereza ni jambo la kawaida. Viongozi wa Serikali wanajifanya miungu watu. Akina Mbowe tukinyamaza mtapigwa viboko barabarani,”alisisitiza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu, alisema misukosuko anayopitia Mbowe kisiasa na kibiashara inazidi kumpa ujasiri wa kupigania haki. “Hata dhahabu ili ing’ae ni lazima ipitie kwenye moto na ndio maana Mbunge wenu anapitia misukosuko mingi lakini imemuimarisha na kumpa ujasiri zaidi,”alisema Kiwelu.
Mwenyekiti wa Baraza la Halmashauri ya Hai (Chadema), Helga Mchovu aliwaomba radhi wananchi wa kata ya Mnadani kutokana na kitendo cha diwani wao kuwakimbia na kuwaacha yatima.
No comments:
Post a Comment