Translate
Tuesday, December 26, 2017
SERIKALI YASHAULIWA KUMALIZA TATIZO LA AJILA KWA VIJANA
Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kuweka mikakati kumaliza tatizo la ajira kwa vijana na ambao wameshindwa kujiunga na elimu ya juu kwa kukosa mikopo.
Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao amesema hayo Jana Desemba 25,2017 wakati wa misa ya Krismasi ambayo kitaifa kwa kanisa hilo imefanyika jimboni humo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Minara Miwili.
Amesema Serikali inapaswa kushughulikia kero za watu wanaoteseka na hasa vijana ambao wamemaliza masomo lakini hawana ajira na walioshindwa kujiunga na vyuo vikuu kwa kukosa mikopo.
Amesema suala la kuhimiza vijana kujitahidi kwenye masomo linahitaji kwenda sambamba na kuwapatia ajira kwa kuwa wengi wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini.
“Tuliwahimiza vijana wasome, wakasoma kwa bidii na kufaulu vizuri, wengi wa hawa wametoka katika familia zenye kipato cha chini, maelfu wanazurura mitaani wanashindwa kuingia vyuoni kwa kukosa ada,” amesema.
Amesema kama jitihada zisipofanyika kwa kuwapa kipaumbele vijana katika kuwapatia mikopo, kutakosekana wataalamu wa kuendana na mazingira ya sasa na hasa katika viwanda.
Wakati huohuo, Askofu Shao amevikumbusha vyama vya siasa kuwa njia ya kumaliza tofauti ni mazungumzo.
“Tukubaliane kutofautiana na kuheshimu tofauti zetu, sababu za Watanzania kukubali kuwa na vyama vingi vya siasa ni kutaka kutoa changamoto kwa maswali ya msingi ya maendeleo, kufichua maovu na udhaifu wa Serikali,” amesema.
Amesema vyama vingi vinasaidia kuleta uwazi katika Serikali hivyo ni vyema kuheshimu tofauti zinapojitokeza.
Kuhusu ukwepaji wa kodi, alisema kufanya hivyo ni dhambi kwa sababu kunaathiri kizazi cha sasa na kijacho na jamii kukosa huduma.
“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya jamii, suala la ulipaji kodi ni haki na lazima,’’ amesema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment