Translate

Wednesday, May 18, 2016

UTUMBUAJI MAJIPU WAMGEUKIA MAGUFULI






Dk. John Magufuli, Rais wa Tanania

Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania
DHANA ya utumbuaji majipu sasa imemgeukia Rais John Magufuli kutokana na kuongoza wizara iliyotawala na ubadhirifu wa fedha za umma, anaandika Regina Mkonde .
Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imemtaka Rais Magufuli kutumbua majipu yake wake wakati akiwa kwenye wizara hiyo.
James Mbatia, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema, katika wizara hiyo kuna ubadhilifu wa fedha za umma
.
Pia kumekuwepo na utendaji mbovu wa watumishi na kwamba, serikali haina mpango wa kuwachukulia hatua za kisheria wahusika kutokana na kutoonesha jitihada.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inajiuliza kama  serikali ya awamu ya tano inafanya kazi yake kwa haki, uadilifu, uwazi na usawa kwa wote na hasa kwa kile kinachojulikana kama utumbuaji majipu, swali hapa ni nani amfunge paka kengele? au mkuki mtamu kwa nguruwe mchungu kwa binadamu?” amehoji Mbatia.
Wakati akitoa hotuba ya maoni ya kambi ya upinzani leo Bungeni mjini Dodoma kuhusu mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 Mbatia amefafanua baadhi ya dosari zilizofanywa na wizara hiyo.
Moja kati ya dosari hizo ni kitendo cha Wakala wa Barabara nchini TANROADS cha kuitia hasara zaidi ya Sh. 5 bilioni serikali.
“TANROADS imebainika kuwa na utendaji mbovu kama ambavyo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) alivyobaini juu ya usimamizi mbovu katika mikataba ya ujenzi wa barabaa na madaraja ambapo ilikuwa chini ya iliyokuwa wizara ya ujenzi katika serikali ya awamu ya nne,” amesema.
Mbatia ameongeza kuwa “TANROADS wakati wa kipindi hicho, iliitia hasara serikali ya jumla ya Shilingi 5,616,652,051 kutoka kwenye riba (interest) inayoongezeka kila siku kutokana na TANROADS kuchelewa kuwalipa wakandarasi 11.”
Amesema kuwa, hasara hiyo iligundulika kati ya kipindi cha mwaka 2012 na mwaka 2015 kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya Hesabu za Serikali Kuu wakati wa ukaguzi wa taarifa za fedha kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2015 iliyotolewa mwezi Machi 2016 (Ukurasa wa 134 na 135).
Dosari nyingine ni ile ya serikali kuruhusu matumizi ya matairi yanayofahamika kwa jina la Super single tires ambayo yanaharibu barabara.
“Utafiti unaonesha matairi haya (super single tyres) yanaharibu barabara. Matairi haya yameanza kutumika takribani miaka mitano iliyopita na mzigo uliokuwa unabebwa na matairi 24 sasa unabebwa na matairi 12,” amesema.
Mbatia amesema, uruhusiwaji wa matumizi ya matairi hayo haukuwa wa busara kutokana na kwamba matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa barabara.
“Uamuzi wa kuruhusu matairi haya haukuwa na busara maana barabara zetu hazijabuniwa kuhimili shinikizo la uzito (excessive pressure) linalotokana na matairi hayo,” amesema.
Ameitaka serikali kuzuia mara moja matumizi ya matairi hayo ili kuzinusuru barabara lakini pia kuokoa fedha za walipa kodi zinazotumika kurekebisha mara kwa mara barabara hizo na kunyima fursa maeneo mengine kupata barabara za kiwango cha lami.
Akizungumzia uuzwaji wa nyumba za serikali Mbatia amesema, serikali iliuza nyumba zake kwa bei ya hasara hivyo kuigharimu nchi.
“Katika muktadha huo kambi Rasmi ya Upinzani  inalikumbusha Bunge kwamba, kati ya mwaka 2002 mpaka 2004  Serikali iliuza nyumba  zipatazo 7,921 na mpaka mwaka 2008 Serikali ilikuwa imejenga nyumba 650 tu,” amesema.
Amesema kuwa, katika biashara ya kuuza nyumba zilizokuwa mali ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), serikali ilipata Sh. 252,603,000/-
ambazo haziendani na thamani halisi ya nyumba hizo.
“Hivi sasa serikali inahitaji kusaka nyumba  zaidi ya mara dufu ya kiasi hicho kujenga nyumba za fidia.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya uuzaji wa nyumba za serikali kinyume cha taratibu, serikali itatumia Sh. 677,606,000/- kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe kwa Tamisemi, Rejea taarifa ya Serikali Bungeni tarehe 25 April 2008,” amesema.
Mbatia amesema, waliouziwa nyumba hizo, kuna taarifa kuwa kati yao wapo walioziuza na kujipatia faida kubwa kinyume na mikataba ya mauzo hayo,na kwamba KRUB inapendekeza wanyang’anywe nyumba hizo kwa kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.
“Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge zinaonesha kwamba, serikali ilitoa taarifa ndani ya Bunge hili kuwa, kuna kamati iliundwa kuchunguza mchakato wa mauzo ya nyumba ya serikali.
“Kamati hiyo ilitegemewa kumaliza kazi mwezi Februari, 2007, lakini hadi Bunge la Tisa na Bunge la Kumi linamaliza uhai wake hakuna taarifa iliyotolewa na serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani Buneni inaitaka serikali ya awamu ya tano irejeshe nyumba hizo,” amesema.
Mbatia amesema, kuna maadhimio kadhaa yaliyoadhimiwa na bunge ikiwemo kuitaka serikali kurejesha nyumba zilizouzwa kinyume cha taratibu na kwa watu ambao hawakuwa watumishi wa umma.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeiitaka Serikali kutekeleza azimio hilo la Bunge, na kwa njia hiyo ile kauli mbiu ya hapa kazi tu, iweze kutafsiriwa kwa vitendo,” amesema na kongeza;
“Tunajua uuzwaji huo ulisimamiwa na Wizara aliyokuwa akiiongoza yeye na kuna uwezekano mkubwa kwamba alisimamia maamuzi ambayo hakuwa na uwezo wa kuyakiuka.”
Amesema, sasa ni muda sahihi Rais Magufuli kurekebisha kasoro alizozisimamia na katika mchakato huo ili kurejesha imani katika jamii.
“Tukumbuke kuwa Rais Kikwete alielekeza nyumba hizo zirudishwe serikalini lakini alikosa uthubutu wa kusimamia kauli yake,” amesema.
Credit :- Mwanahalisi online

No comments:

Post a Comment