Bodi ya Wadhamini ya CUF kupitia wakili wao, Hashimu Mziray leo imewasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuazi uliotolewa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu uliotupilia mbali kesi yao sababu CUF haina Bodi ya wadhamini.
Bodi hiyo inapinga uamuzi wa uliotolewa mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambapo maombi yao dhidi ya Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma(CUF) na wenzao sita yakuomba mahakama iwazuie kwa muda kujihusisha katika masuala ya uongozi na kufanya mikutano ya chama.
Wakili wa bodi ya Wadhamini ya CUF, Hashimu Mziray amesema wamewasilisha kusudio hilo la kukata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na hakimu Mashauri kwa kuwa si kweli kuwa CUF haina bodi ya wadhamini.Amedai kuwa CUF IPO hai, inawabunge, madiwani, majengo, wanachama na kwamba msajili wa vyama vya siasa hajakifuta.
ameongeza Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri hakulielewa tangazo la Wakala wa Vizazi na Vifo (Rita) na kuiomba Mahakama Kuu itengue maamuzi ya Hakimu Mashauri kwa kuwa ni batili.Mei 21 mwaka huu, Hakimu Mashauri alitoa uamuzi wa kuitupilia mbali kesi hiyo baada ya kusikiliza pande zote mbili.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema Joram Bashange ambaye aliapa katika kiapo kuwa ni Katibu wa Bodi ya Wadhamini ya CUF aliapa uongo kwa sababu bodi hiyo ilisha isha muda wake na kwamba pande zote mbili wana maombi RITA ya kuomba usajili.ameongeza kuwa Bashange ni Katibu wa Bodi ya Wadhamini ya CUF na kwamba yeye binafsi ndiye atabeba gharama za kesi.
Katika kesi hiyo Sakaya na wenzake walikuwa wakiwakilishwa na Wakili, Mashaka Ngole huku bodi ya Wadhamini ya CUF ikiwakilishwa na Wakili Hashimu Mziray.
Katika pingamizi wajibu maombi wanadai maombi hayawezi kusikilizwa katika mahakama hiyo kwa sababu yanashughulikiwa katika maombi namba 23/2016 yaliyopo Mahakama Kuu.Wanadai mwombaji hana miguu ya kusimamia kufungua kesi dhidi ya wajibu maombi, maombi hayo hayana msingi kwa kushindwa kubainisha jina la mwandishi wa masuala ya fedha hivyo wanaiomba mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo kwa gharama.
Maombi hayo yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura ni dhidi ya wajibu maombi Sakaya, Nachuma, Thomas Malima, Omar Masoud, Abdul Kambaya, Salama Masoud, Zainabu Mndolwa na Jaffari Mneke.
Bodi ya wadhamini ilikuwa inaomba mahakama itoe zuio la muda kuwazuia wajibu maombi, mawakala wao au watu wao wowote kujihusisha katika masuala yoyote ya uongozi au kufanya mikutano ya chama hicho, hadi maombi yao hayo yatakaposikilizwa kwa pande zote husika.Wakili Mziray aliomba maombi hayo yasikilizwe kwa haraka kwa madai kwamba wajibu maombi wanataka kujiingiza katika kufanya mikutano ya chama hicho, wakati hawana uwezo wa kufanya hivyo.
Bodi hiyo ya wadhamini ya CUF iliamua kufungua kesi hiyo mahakamani hapo siku moja baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba, kutangaza kutengua nafasi tano za wakurugenzi wa chama hicho na kutangaza majina mapya.
No comments:
Post a Comment