Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi wakati huo, Patrick Chokala
Dar es Salaam. Siku mbili zikiwa zimepita tangu Dk Louis Shika kuelezea siku 28 za mateso aliyoyapata nchini Urusi, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo wakati huo, Patrick Chokala amefichua siri jinsi walivyomsafirisha kijasusi ‘bilionea huyo wa nyumba za Lugumi’ kurudi Tanzania.
Balozi Chokala aliyekuwa Urusi kati ya mwaka 2002 na 2008 katika kipindi ambacho sakata la utekwaji wa Dk Shika lilijitokeza, amethibitisha kuwa ni kweli Mtanzania huyo ni daktari na kwamba ni kweli amewahi kutekwa.
Dk Shika anatuhumiwa kuvuruga mnada wa majumba ya mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi uliofanywa na kampuni ya Yono baada ya kufika bei ya kuzinunua nyumba hizo tatu kwa Sh3.2 bilioni, lakini akashindwa kutimiza sharti la kulipa asilimia 25 ya fedha hizo.
Kushindwa huko kulipa kulisababisha awekwe rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa siku sita hadi alipoachiwa kwa kujidhamini mwenywe Novemba 14 na kutakiwa kuripoti kila siku.
Mara baada ya kutoka polisi kwa dhamana, Mwananchi lilifanya mahojiano maalumu na Dk Shika nyumbani kwake Tabata Mawenzi na alieleza mambo mbalimbali ikiwamo kutekwa na kuteswa akiwa Urusi Juni 2004, ikiwa ni pamoja na kukatwa vidole viwili mkono wa kushoto na kimoja mkono wa kulia.
Pia alieleza jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka watekaji hao.
Jana, Mwananchi lilizungumza na Balozi Chokala ambaye alisema analikumbuka vizuri tukio la kutekwa kwa Dk Shika na jinsi ubalozi ulivyomsaidia asipatwe na kadhia kubwa zaidi. “Ni kweli huyo jamaa ni daktari wa binadamu. Alisoma Chuo Kikuu cha Lumumba kilichopo Moscow, Urusi,” alisema Balozi Chokala.
Alisema kutokana na upekee wa yaliyomsibu Dk Shika, ubalozi ulilazimika kuingilia kati ili kunusuru maisha yake.
Kwa kumbukumbu zake, balozi huyo alisema Dk Shika alitekwa na majambazi waliokuwa wanataka fedha ambazo yeye mwenyewe (Dk Shika) alikuwa anajigamba kuwa nazo na kuwashawishi watekaji hao kumfuatilia. “Majigambo ya kumiliki fedha nyingi hajayaanza leo. Tangu akiwa Urusi alikuwa anasema anamiliki fedha nyingi. Watu walimuamini kwa sababu alikuwa daktari anayetambulika, matokeo yake alitekwa,” alisema Chokala, ambaye amewahi kuwa mwandishi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Balozi huyo alisema baada ya kufanikiwa kuwatoroka majambazi hao ambao baadaye walikamatwa na polisi nchini humo kisha kufunguliwa mashtaka, Dk Shika alipelekwa hospitali kwa matibabu akiwa amepoteza vidole kadhaa vya mikono yote miwili.
Alisema majambazi hao walimtesa kwa muda mrefu kwa kuwa mpaka anapatikana vidole hivyo vilikuwa vimeanza kuoza.
“Walimshikilia kwa muda mrefu kwa kuwa walihitaji fedha ambazo Dk Shika hakuwa nazo,” anakumbuka balozi huyo aliyestaafu mara baada ya kurudi nchini.
Alisema baada ya ubalozi kupewa taarifa zake, ulifuatilia na kugundua kwamba alipelekwa nchini humo na Wizara ya Afya, na alikuwa amelipiwa kila kitu ikiwa ni pamoja na tiketi ya ndege.
Wakati anatekwa, alisema Dk Shika alikuwa ameshahitimu lakini hakuwa na nauli ya kurudi nyumbani, hivyo akawa anahangaika kupata nafasi ya kuendelea na shahada ya uzamili. “Tulipowasiliana na wizara walithibitisha kuwa ni mtu wao. Tuliandaa utaratibu wa kumrudisha bila yeye kujua kwa sababu hakuwa anataka kufanya hivyo,” alisema.
Akiwa anaendelea kuhudumiwa, ubalozi ulimuandalia safari ya kurudi bila yeye kufahamu kuepuka asitoroke. Balozi Chokala alisema ilikuwa ni lazima Dk Shika arudishwe kuepusha janga jingine linaloweza kumkuta endapo angeendelea kuishi nchini humo. “Kujirudia kwa tatizo kama hilo kungeupa ubalozi lawama. Hatukutaka kujiweka kwenye nafasi hiyo,” alisema.
Baada ya mipango yote kukamilika, askari wa ubalozini walimpeleka uwanja wa ndege na kumkabidhi kwa wahudumu wa ndege iliyokuwa inakuja Tanzania wakiwaelekeza wasimshushe popote isipokuwa Dar es Salaam ambako Wizara ya Afya ilikuwa inamsubiri.
Mpango huo ulitekelezwa kama ulivyopangwa na wizara ikathibitisha kumpokea mtumishi wake huyo ambaye balozi Chokala anasema alipewa nyumba na akawa anaendelea na majukumu yake. “Akiwa Urusi, nilielezwa kuwa alikuwa ana matatizo ya kijamii ambayo yaliendelea kumuandama hata aliporudi. Nasikia kuna wakati alienda kwao na hakurudi tena kazini,” alisema.
Kwa muda wote wa kushughulikia sakata la ‘bilionea’ huyo, balozi alisema hakuonana naye na alipomsikia kwenye vyombo vya habari akawa hana uhakika ingawa jina lilikuwa lenyewe. “Siwezi kumsahau. Tukio lake lilikuwa la kipekee,” alisema na kufafanua kuwa ubalozi haukuendelea kufuatilia kesi yake kwa kuwa walichokipa kipaumbele ni usalama wa Mtanzania huyo.
Kuhusu Dk Shika kuwa ni Rais wa kampuni ya Lancefort aliyoianzisha akiwa Urusi ambayo Serikali ya nchi hiyo ilitilia shaka mwenendo wake, hivyo kuifuatilia, Balozi Chokala alisema hafahamu chochote.
“Siwezi kulizungumzia hili. Kwa wakati huo, usalama wake ulikuwa muhimu zaidi na ndio tulioupa kipaumbele,” alisema.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment