ASKARI Polisi zaidi ya 10 waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi, hivi karibuni walivamia hoteli aliyofikia mgombea ubunge wa jimbo la Bunda Mjini (Chadema) na kuanza kumpekua na watu wengine waliofika hotelini hapo. Anaandika Moses Mseti, Bunda … (endelea).
Tukio hilo lilitokea Septemba 9 saa 3:00 usiku wakati askari hao walipofika hatolini na kuanza upekuzi huku askari wengine wakiwa wameizingira hoteli hiyo waliokuwa na silaha (SMG) na mabomu ya machozi.
Hata hivyo katika tukio hilo ambako askari wengine walionekana wakiwa wamevalia sare polisi wengine kiraia wakiwa wamejaza mabomu ya machozi katika miili yao kitendo ambacho kilionesha kuwatisha na kuwakera wageni waliokuwa hotelini hapo.
Katika upekuzi huo uliofanyika hadi sa 4:30 usiku, askari hao hawakufanikiwa kumkamata mtu yeyote wala kusababisha uvunjifu wa usalama kwa mgeni na watu wengine waliokuwa nje karibu na hoteli hiyo.
Askari mmoja akizungumza na Mwanahalisi Online, kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini alisema kufanyika kwa upekuzi huo kunatokana na kuwepo kwa taarifa kuna vijana waliohifadhi mapanga kwenye hotelini hapo.
Amesema licha ya kupata tarifa hizo za kuwepo na vijana wenye mapanga ambako hakutaja lengo la kuhifadhiwa kwake, alidai wamefanya upekuzi, chumba hadi chumba na hakuna walichoambulia.
“Kumbe taarifa tulizopewa ni za uongo na kuzushwa tuu mtaani, tunaomba samahani kwa usumbufu mlioupata, ni lazima ufanyike upekuzi kuweka usalama sawa,” alisema askari huyo.
Akizungumzia hali hiyo, Bulaya ambaye alifikia hoteli hiyo kwa lengo la kuendelea na mikutano yake ya kampeni, alidai kuwa askari hao kufanya upekuzi huo ni njama za CCM za kutaka kumkatisha tamaa na kwamba hawataweza.
Amesema wananchi wa Bunda wameishaichoka CCM na rangi zao na makopo yao (wagombea wao) hivyo ndiyo maana wanatumia mbinu hizo ili kuwakatisha tamaa na kamwe mbinu hizo hazitafanikiwa, kumrudisha nyuma katika harakati za kulikomboa Taifa.
Hata hivyo Bulaya hivi karibuni alichukuliwa na jeshi la Polisi wilayani humo kwenda kumhoji, mara baada ya kutoka amesema Mkuu wa Polisi Wilaya OCD, alionekana akipendelea upande mmoja wa CCM.
Bulaya ambaye anaoeneka kuungwa mkono na wananchi wa jimbo hilo hususani vijana na wanawake, amekuwa akimshambulia waziri wa Kilimo na Ushirika, Steven Wassira kwa kushindwa kuwatatulia kero zao, hiyo ndiyo inaelezwa kuwa chanzo za kufanyiwa fitina hizo.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kung`ombe na kuhudhuliwa na mamia ya wananchi, amesema Wassira ameshindwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Bunda, ikiwemo tatizo la maji ambalo limekuwa `sugu` jimboni humo.
No comments:
Post a Comment