SIKU moja kabla ya kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) kimepanga kubadilisha upepo, anaandika Faki Sosi.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba, CUF ambayo tayari imeweka msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi huo haramu ulioitishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (CUF) tarehe 20 Machi mwaka huu, kimepanga kuushangaza ulimwengu tarehe 19 Machi mwaka huu.
Taarifa hizo zinaeleza kwamba, pamoja na harakati zinazofanywa na Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ZEC na baadhi ya vyama vichanga viswani humo kushiriki uchaguzi, CUF imeonekana kutoyumba katika msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi huo.
Akithibitisha taarifa hizo, Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF amesema, chama hicho kitatoa tamko zito siku hiyo.
“Kinachoendelea kwa sasa Zanzibar hatushughuliki nacho, waendelee na mipango yao lakini tarehe 19 chama kitatoa tamko,” amesema Kambaya na kuongeza“chama hakiyumbi hata kidogo.”
Kwa muda mrefu sasa wanasiasa, wachambuzi, jamii na mataifa ya nje wamekuwa yakionya hatua iliyochukuliwa na Jecha Salim Jecha, kada wa CCM kupitia mwavuli wa uenyekiti wa ZEC kuwa, kuvuruga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 25 Machi mwaka jana kunaweza kusababisha mauaji.
Kada hizi mara kadhaa zimekuwa zikimtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na mkwamo wa kisiasa visiwani humo jambo ambalo amelipuuza.
Akizunumza na wazee wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Magufuli alieleza kwamba ‘siingilii’ uchaguzi huo licha ya kutakiwa kufanya hivyo.
Katika kuonesha kilele cha kupuuza ushauri huo, Rais Magufuli alisisitiza kwamba, kwa kuwa yeye ndiye amiri jeshi mkuu, atawashughulikia watu wowote ‘watakaoleta fyokofyoko’ kauli iliyotafsiriwa kuwatisha wazanzibari wanaopinga marudio ya uchaguzi.
Licha ya kauli za vitisho kutoka kwa Rais Magufuli, hali ya wasiwasi inaendelea kutawala visiwani Zanzibar hasa baada ya wananchi, CUF na vyama vingine tisa kutotikisika.
CCM kilikuwa chama cha kwanza kusherehekea hatua ya Jecha kufuta uchaguzi wa Oktoba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment