Translate

Monday, August 29, 2016

LOWASSA, MBOWE, MASHINJI NA MNYIKA WAVAMIWA NA POLISI

VIONGOZI wandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamekamatwa na jeshi la polisi wakati wakiendelea na kikao chao cha Kamati Kuu (CC), kwenye hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam, 

Taarifa zinasema, katika kamatakamata hiyo, mtafaruku mkubwa ulizuka baada ya viongozi wa jeshi hilo kutaka Chadema, kusitisha kikao chake cha CC, kilichokuwa kikiendelea hoteli hapo.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinasema, baada ya mabishano makali, jeshi la polisi liliamuru baadhi ya viongozi wa chama hicho, kufika makao makuu ya polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.
Waliotakiwa kufika makao makuu ya polisi, ni pamoja na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe; mjumbe wa Kamati Kuu na waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa; Katibu Mkuu, Vicenti Mashinji na naibu katibu mkuu (Bara), John Mnyika.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Mwita Mwaikabe Waitara, amethibitishia MwanaHALISI Online, kuitwa kwa viongozi hao na kusema, “kwa sasa tuko njiani tunaekelea Central (polisi kati), kufuatilia kinachoendelea.”
Waitara ambaye ni mbunge wa Ukonga amesema, “polisi wametaka tughairishe kikao chetu cha Kamati Kuu, kwa madai kuwa mikutano na vikao vya ndani vimezuiwa. Lakini tumekataa na hilo limetufanya tuwe na nguvu zaidi ya kufanya maandamano na mikutano, 1 Septemba.”
Mkutano wa kamati kuu ya Chadema, umeitishwa ili kujadili ufanikishaji wa maandamano hayo.
Kukukamatwa kwa viongozi wakuu wa Chadema na kutakiwa kuripoti polisi kwa mahojiano, kumekuja wakati viongozi wa madhehebu ya kidini wakiomba serikali kuruhusu kufanyika kwa mikutano na maandamano ya upinzani.
“Viongozi wa madhehebu ya kidini wamenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari wakishauri serikali kuruhusu upinzani kuandamana na kukutana kwa kuwa suala hilo, limeruhusiwa kwa mujibu wa katiba.
Jeshi la polisi limekuwa likifanya maandalizi ya kutumia virungu, silaha za moto, maji ya washawasha, mbwa na risasi za plastiki, kuzuia maandamano ya upinzani.
Chadema imeitisha maandamano na mikutano nchini mzima, tarehe 1 Septemba, kama sehemu ya uzinduzi wa Operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta nchini (UKUTA).
Katika waraka wake uliosambazwa kwa viongozi wa wilaya, majimbo, mikoa na kanda, chama hicho kimetaja vitendo kadhaa, ikiwamo marufuku ya mikutano ya hadhara na kuzuiwa kwa urushaji wa matangazo ya Bunge, kuwa ni “miongoni mwa dalili za nchi kuelekea kwenye utawala wa kidikteta.”
Maeneo mengine iliyosema yanaashiria utawala wa kiditeta, ni kudhibiti wabunge wa upinzani bungeni, kuingiliwa kwa uhuru wa mahakama, kupuuzwa kwa utawala wa sheria, uhuru wa kujieleza na kufutwa kwa uchaguzi mkuu huru na haki wa 25 Oktoba, Visiwani.
Kuhusu uhuru wa mahakama, waraka unatoa mfano wa hatua ya Rais Magufuli, kuelekeza wafanyabiashara wanaotuhumiwa kukwepa kodi, kuhukumiwa haraka na kuahidi kutumia sehemu ya fedha itakayopatikana kutoka kwa wafanyabiashara hao, kuipa mahakama.
Maandamano na mikutano ya Chadema imepigwa marufuku kwa tangazo la Rais John Pombe Magufuli alilolitoa mkoani Singida, Julai mwaka huu, ambako alitamka waziwazi kuwa wanaotaka kufanya siasa wasubiri hadi mwaka 2020.
Alisema muda wa siasa uliisha baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kwamba sasa anahitaji muda kutekeleza alichowaahidi wananchi; akiongeza kuwa chama kinachopaswa kuzunguka nchi kushukuru wananchi ni kile kilichoshinda.
Alisema, “sijawahi kujaribiwa na sijaribiwi.” Aliwataka wanaotaka kufanya mikutano na maandamano kutangulia mbele ili naye aweze kuonyesha nguvu ya vyombo vyake vya dola.
Rais alijihalalisha pekee kuwa mwenye sababu ya kuzunguka nchi nzima – kila jimbo – kufikisha maendeleo aliyowaahidi Watanzania wote.
Kwa mujibu wa Waitara, polisi walivamia mkutano huo na kuagiza ufungwe.
Katika hatua nyingine, Waitara amewataka viongozi wa Chadema jijini Dar es Salaam na maeneo jirani, wanachama na wafuasi kujitokeza kwa wingi makao makuu ya polisi ili kuhakikisha viongozi wao waliokamatwa wanaachiwa na mikutano na maandamano inafanyika kama ilivyopangwa.
“Ndugu viongozi, kikao cha Kamati Kuu kimeghairishwa baada ya polisi kuvamia mkutano wetu. Hivi sasa, tunaelekea makao makuu ya polisi, hivyo tunawaomba mjitokeze kwa wingi kupinga udhalimu huu,” anaeleza.
Anasema, “hii ni kwa wote wanaopenda utawala bora na demokrasia ya vyama vingi nchini. Hatuwezi kukubali kunyanyaswa na kuendesha taifa kwa njia hii.”
Amesema, “naowamba wananchi wa jimbo langu la Ukonga na majimbo mengine yenye wabunge wa upinzani; naziomba halmashauri zetu za jiji la Dar es Salaam, kujitokeza haraka polisi makao makuu kuhakikisha haki inatendeka.”

No comments:

Post a Comment