Mwili wa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline umepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo Jumatatu Februari 19,2018 asubuhi.
Mwili wa Akwilina umehamishiwa Muhimbili ukitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Ndugu wa marehemu wamekusanyika Muhimbili katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti, wakisubiri uchunguzi ukamilike ili kujua hatima ya kuusafirisha kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
Akwilina alifariki dunia Februari 16,2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala na polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.
Akizungumza na MCL Digital hospitalini Muhimbili leo Februari 19,2018, Moses Kiyeyeu aliyejitambulisha kuwa ni kaka wa marehemu amesema madaktari na wahusika wengine wanaendelea na utaratibu wa uchunguzi wa mwili.
"Mwili umefikishwa hapa tangu asubuhi na kule ndani kuna kaka yetu ndiye anashuhudia uchunguzi huo, wametwambia tutoke kwanza ndani watatuita baadaye ili kupewa taarifa nini kinafuata kuhusu mwili wa ndugu yetu," amesema.
Kiyeyeu amesema familia inasubiri uchunguzi ukamilike ili waruhusiwe kuuchukua mwili kwa kuwa wazazi wa Akwilina wanausubiri.
No comments:
Post a Comment