Translate

Monday, October 19, 2015

MBOWE AHAMISHA MABILIONI KINYEMELA

Wasifu wa Afisa wa Benki Junaid Ali, Bonyeza Hapa 

Atumia makampuni ya Dubai na Hong KongKahongwa na Lowassa?

WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akituhumiwa  kuhongwa ili kumpitisha Edward Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho, imefahamika kwamba amefanya uhamisho wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti yake hivi karibuni.

Mbowe, ambaye uamuzi wake wa kumpitisha Lowassa kuwania urais pasipo kushindanishwa na mtu ndani ya chama chake na ndani ya muda mfupi unadaiwa kukigawa chama hicho, amefanya uhamisho huo wa fedha kwa kumtumia mtu anayeitwa Junaid Ali, ambaye ni Meneja wa Mahusiano ya Wateja wa Benki ya Noor iliyopo Falme za Kiarabu.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai anayemaliza muda wake, ana makampuni mengi hapa nchini lakini amefanya uhamisho huo wa fedha kwa kutumia kampuni isiyofahamika sana ijulikanayo kwa jina la Aretra World Wide Limited.

Kwa kumtumia Ali, Mbowe aliagiza fedha hizo zipelekwe katika akaunti tatu tofauti ambazo zote ziko nje ya Tanzania.

Kampuni hizo na kiasi cha fedha kilichopelekwa ni Puku Hong Kong Limited iliyotumiwa dola 230,555 (shilingi milioni 461), TanChin Trading Co. Limited iliyotumiwa dola 302,614 (shilingi milioni 605) na Hong Kong Da Web International Tradings Limited  iliyotumiwa dola 489,860 (shilingi milioni 980). Jumla ya fedha zote zilizohamishwa ni zaidi ya shilingi bilioni mbili.

Makampuni yote yaliyotumiwa fedha yana ofisi zake nchini Hong Kong na yote yamefunguliwa akaunti katika benki maarufu ya HSBC.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba Junaid Ali ambaye amepewa maelekezo ya kufanya malipo hayo ni mtaalamu wa masuala ya kufungua makampuni yanayojulikana kama offshore ambayo mara nyingi hutumiwa na wafanyabiashara kufanya malipo pasipo kujulikana na watu.

Makampuni ya namna hii hufunguliwa katika nchi zenye usiri mkubwa kwa watu wanaohifadhi fedha na ndiyo maana wakati wa sakata la ununuzi wa rada, Andrew Chenge na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Idris Rashid, walitumiana fedha kupitia akaunti zao zilizo katika nchi zinazoongoza kwa kuwa na makampuni mengi ya namna hii.

Akimwandikia Junaid, Mbowe alisema; “ Tafadhali, nakuomba na kwa haraka, ufanye uhamishaji wa fedha kutoka katika benki yako na kwenda kwenye akaunti zifuatazo; Puku, TanChin na Hong Kong Da Web,” aliandika Mbowe.

Katika barua hiyo ambayo gazeti hili imefanikiwa kuona nakala yake, Mbowe ameitambulisha kampuni yake kwa anuani ya S.LP 293816, iliyopo katika jengo la World Trade Centre, Mtaa wa Sheikh Zayed, Dubai.

Uhamisho huo mkubwa wa fedha umefanyika katika kipindi ambacho wagombea ubunge wa chama hicho wamelalamika kwamba wamekosa msaada wa chama chao kifedha; huku kukiwa na tuhuma kwamba huenda viongozi wa juu wa Chadema; hasa Mbowe, walihongwa fedha ili kumruhusu Mbowe awanie urais.

Tayari, mmoja wa washauri wa siasa wa Chadema kutoka Marekani, Joe Costello, amewaandikia waraka viongozi wa juu wa Chadema, akisema kwamba asilimia 30 ya wana Chadema wamechukizwa na uamuzi wa Lowassa kuchaguliwa kuwa mgombea katika mazingira yanayozua maswali na hawamtaki.

Kwa kuwa kampuni hiyo ya Mbowe ni offshore, gazeti hili limeshindwa kufahamu ni kiasi gani cha fedha Mbowe amehifadhi au ameweka kwenye akaunti hiyo na chanzo cha mapato hayo ni kipi kwa vile biashara zake nyingi anafanya hapa nchini, ingawa ameanza kujitanua kimataifa.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba Mbowe alitakiwa kupokea kiasi cha dola 330,000 (shilingi milioni 660) –takribani sawa na fedha aliyoihamishia TanChin Hong Hong, kutoka kwa wafadhili wa chama hicho waliopo nchini Japan.

Kwa mujibu wa mawasiliano baina ya viongozi wa juu wa Chadema na wafadhili hao wa kijapani kupitia kwa mtu anayefahamika kwa jina la Naomi pamoja na Mchungaji Mariko Morikubo, Chadema ilikuwa ichangiwe fedha za kijapani (Yen), milioni 40 ambazo ni sawa na dola 330,000 kabla ya mwisho wa Julai mwaka huu.

Mawasiliano ya awali baina ya wafadhili hao ambao ni makanisa ya Kikristo yaliyoko nchini Japan, yalianzishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, ambaye aliomba msaada wa magari pamoja na fedha kwa ajili ya kusaidia Chadema kwenye uchaguzi huo.

Ndani ya Chadema, ni viongozi wakuu watatu ndiyo wanaonekana kushiriki katika mazungumzo hayo; Mbowe, Slaa na Reginald Munisi ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho.

Barua pepe za awali kutoka kwa Slaa kwenda kwa akina Naomi wa Japan zinaonekana kuanza kuandikwa mwanzoni mwa mwaka huu, lakini Mbowe aliingilia kati ulipofika wakati wa kupokea malipo.

Akiandika kupitia barua pepe ya Jumatatu, Aprili 20, 2015, Mariko aliwataka viongozi wa Chadema kumpa taarifa muhimu kuhusu namna atakavyofanya malipo, namba ya akaunti ya Chadema pamoja na mambo mengine.

“ Salamu kutoka Japan. Takaboshi (wafadhili hao wa Chadema) wanakutana kesho jijini Tokyo, Japan. Wanajadiliana kuhusu suala la kuwatumia fedha. Tafadhali naomba namba ya akaunti yenu ya benki ya chama ili wafahamu namna ya kuwatumia,” ilisema barua pepe (email hiyo).

Barua pepe hiyo iliandikwa saa 3:32 asubuhi na ilipofika saa 9:29, Munisi aliijibu lakini badala ya kuwapa akaunti ya Chadema kama wafadhili hao walivyotaka, yeye aliwapa nambari ya akaunti binafsi ya Mbowe.

“ Mpendwa Mariko, nakushukuru sana kwa ufuatiliaji wako. Namba ya akaunti ni 02J1039056202. Jina la mwenye akaunti ni Freeman Mbowe. Au mnaweza kufanya hivyo kwa kutumia akaunti dada ya benki ya Citibank ya Marekani iliyopo jijini New York. Namba ya akaunti hiyo ya fedha za kigeni (dola ya Marekani) ni 36072436,” ilisema sehemu ya barua pepe hiyo ya Munisi ambaye wiki iliyopita alifanya mkutano na waandishi wa habari kulalamika kuhusu masuala ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Baada ya kuona Wajapani wanachelewa kutuma fedha, Mbowe alifunga safari yeye mwenyewe kwenda nchini humo kuonana na wafadhili hao kama ambavyo barua pepe aliyowaandikia inavyosema.

“Nimewasili salama hapa Guangzhou, China. Nawashukuru kwa mawasiliano yenu na Dk. Slaa na utayari wenu wa kuniona Tokyo. Sitakuja peke yangu bali nitafuatana na mtu ambaye, kwa bahati mbaya, hatashiriki kwenye mazungumzo yetu. Mungu awabariki sana,” aliandika Mbowe.

Gazeti hili linaendelea na uchunguzi wake kuhusu ni nani hasa alifuatana na Mbowe kwenye safari yake hiyo.

Juhudi za kumpata Mbowe kutoa maelezo kuhusu suala hili ziligonga mwamba kwa vile simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na wasaidizi wake waliopokea walisema alikuwa kwenye mikutano ya kampeni za Lowassa.

Mwisho

A

No comments:

Post a Comment