Translate

Monday, August 15, 2016

UCHAGUZI WA MWAKA JANA HAUKUWA RAHISI - JOHN MREMA

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema uchaguzi wa mwaka jana haukuwa rahisi kwani Ukawa ilipitia katika mitikisiko mitatu.

Mtikisiko wa kwanza ni mchakato wa kumpata mgombea urais wa Ukawa ambao haukuwa rahisi kutokana na hali halisi ya uchaguzi huo, mtikisiko wa kuondoka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwisho ni  kutangazwa kwa matokeo ya urais.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi mwishoni mwa wiki, Mrema amesema mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya Ukawa ulikuwa mgumu kutokana na mazingira yalivyokuwa kwa sababu vyama vya Chadema na CUF, kila kimoja kilikuwa na uwezo kutoa mgombea wa urais.

“Ninakumbuka mara kadhaa tuliwaita waandishi wa habari ili tumtangaze, lakini tuliahirisha kutokana na ugumu uliokuwapo katika mchakato huo,” amesema.

Mrema ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ndogo ya kuandaa mapokezi ya kumkaribisha, Edward Lowassa aliyetoka CCM.

Lowassa alijiengua CCM na kujiunga na Chadema siku chache baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kuwania urais mkoani Dodoma.

Mapema kabla ya jina lake kukatwa, Lowassa alikaririwa akisema hakuna wa kumkata jina lake, na kama akikatwa, kwanini akatwe wakati katika mapambano hakuwahi kushindwa.

Mrema amesema, kabla ya mchakato huo wa kumpata mgombea urais haujatulia, Ukawa ikapata mtikisiko wa kuchomoka kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba na baadaye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa.

No comments:

Post a Comment