Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa maombi ya wabunge wanane wa viti maalumu na madiwani wawili wa CUF na hoja moja kati ya nne za pingamizi dhidi ya maombi hayo ya kupinga kuvuliwa uanachama, ndiyo iliyobeba hatima yao.
Hoja hiyo ni ile iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anayewawakilisha katibu wa Bunge na mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo muktadha wake ni Mahakama kutokuwa na uwezo wa kuingilia Bunge katika utekelezaji wa shughuli zake za kikatiba.
Wabunge hao walifungua maombi Mahakama Kuu wakiomba itoe amri ya zuio kwa Bunge ili wabunge walioteuliwa baada ya wao kuvuliwa uanachama wasiapishwe, kusubiri kusikilizwa na kutolewa uamuzi wa kesi waliyoifungua kupinga kufukuzwa uanachama wa chama hicho.
Maombi hayo yalitarajiwa kusikilizwa juzi na Jaji Lugano Mwandambo, lakini yalikumbana na pingamizi la awali kutoka kwa wajibu maombi, wakiiomba mahakama iyatupilie mbali kwa madai kuwa maombi hayo ni batili, huku wakiwasilisha hoja nne, kuyakosoa, jambo ambalo limeyafanya yabaki njia panda.
Ingawa wajibu maombi wote, yaani Bunge, NEC, Bodi ya Wadhamini wa CUF na wabunge wateule wanaosubiri kuapishwa kwa ujumla waliwasilisha hoja nne za pingamizi, lakini kuna mbili zinazopewa uzito katika uamuzi wa mapingamizi hayo.
Mbali na hoja ya Mahakama kutokuwa na uwezo kuingilia shughuli za Bunge, nyingine inayobeba uzito wa maombi hayo kutupiliwa mbali ni ile ya kutumia kifungu kisicho sahihi katika kufungua maombi hayo.
Kama katika uamuzi wake itatupilia mbali hoja nyingine ikiwamo ya uwezo wa Mahakama na ikakubaliana na hoja ya kutumika kwa kifungu cha sheria kisicho sahihi, basi itayatupilia mbali, lakini watoa maombi wanaweza kurekebisha kasoro hizo na kuyafungua tena.
Lakini kama itatupilia mbali hoja nyingine zote na kukubaliana na hoja ya uwezo wa Mahakama kutoa nafuu wanazoziomba, basi itayakataa maombi hayo na hawatakuwa na nafasi ya kuyafungua tena mahakamani hapo.
Hivyo juhudi zao kutaka kuzuia kuapishwa kwa wabunge hao wateule zitakuwa zimeishia hapo na badala yake watasubiri uamuzi wa kesi yao ya msingi kuhusu uhalali wa kufukuzwa kwao uanachama wa chama hicho.
Wabunge waliovuliwa ubunge ni Miza Bakari Haji, Saverina Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Musa na Riziki Shahari Mngwali, Hadija Salum Al- Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala wakati madiwani ni Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madib.
Wakati wa usikilizwaji wa mapingamizi hayo, Bunge na NEC waliwakilishwa na mawakili wa Serikali wanane wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, wakati CUF na wabunge wateule waliwakilishwa na wakili Mashaka Ngole, huku waombaji wakiwakilishwa na mawakili Peter Kibatala na Omari Msemo.
Msajili amtambua Sakaya
Siku moja baada ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF, upande wa Maalim Seif kuwavua uanachama wabunge wawili kwa madai ya kuendeleza hujuma dhidi ya chama hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji mstaafu Francis Mutungi amesema bado anamtambua Magdalena Sakaya kama kaimu katibu mkuu wa chama hicho.
Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua ni miongoni mwa wabunge waliovuliwa uanachama pamoja na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma.
Hatua ya kuwavua uanachama wabunge hao imekuja siku chache baada ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF la upande wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba kuwavua uanachama wabunge wanne.
Katika barua yake aliyoandika Agosti Mosi, nakala kwenda Spika wa Bunge, Job Ndugai, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa CUF, Sakaya, Maalim Seif na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mutungi alisema hadi sasa ofisi yake haijapokea barua yoyote kutoka CUF inayotengua uamuzi wa kumkaimisha Sakaya ukatibu mkuu.
Akizungumzia hatua hiyo ya Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema, “Maalim Seif amepagawa sijui hajui Katiba au la … Katiba inasema wazi kwamba mwenyekiti Taifa ndiye atakuwa mwenyekiti wa baraza kuu la uongozi.
“Sasa yeye na wenzake wamefanya kikao bila mimi kuwepo hicho kitakuwa siyo kikao na uamuzi wake ni batili na siku ile nilisema baraza kuu la Zanzibar ni ‘feki’,” alisema Profesa Lipumba huku akijitetea kwamba habebwi na Msajili wa Vyama vya Siasa, bali mlezi huyo anafuata Katiba ya CUF na kwamba hawezi kulitambua baraza kuu la uongozi litakaloitishwa na Maalim Seif.
Alisema kwa ilivyo sasa, katibu mkuu huyo hana pa kutokea na mwisho wa siku ataishia kulalamika kwa wananchi kupitia vyombo vya habari jambo ambalo halitamsaidia huku akimtaka kwenda makao makuu ya chama hicho Buguruni kutekeleza majukumu yake.
“Hana namna yule, na Katiba ipo wazi na sisi tunaifuata kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hiki. Lazima na kamati ya maadili imuhoji na vitendo vyake vya kuhujumu CUF,” alisema Profesa Lipumba.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma, Salim Biman alisema kitendo alichofanya Jaji Mutungi ni cha aibu na kusema ukweli utabainika katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na CUF dhidi yake.
No comments:
Post a Comment