Translate

Monday, August 21, 2017

HOFU YAZIDI KUTANDA BONGO MAITI 15 ZAKUTWA KWENYE VIROBA


WAVUVI na wafanyabiashara katika masoko na minada ya samaki ya Kunduchi, Ununio na Feri jijini Dar es Salaam wanaishi kwa hofu baada ya kuwapo kwa taarifa za kuopolewa miili 15 ya watu baharini ikiwa imewekwa katika mifuko maalumu kama viroba, Bara na Zanzibar.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika kilichozungumza na Nipashe, miili hiyo iliokotwa kwa nyakati tofauti na wavuvi ambao waliwajulisha polisi, waliofika kuichukua.

Kuwapo kwa idadi kubwa ya miili inayoopolewa kutoka baharini au kukutwa fukweni ikiwa imefungwa kama mzigo kumefanya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kuingiwa na hofu ya kuja kutakiwa kuisadia polisi katika uchunguzi wa mauaji hayo, pindi wanapogundua na kutoa taarifa za maiti hizo.
Hofu hiyo imesababisha baadhi ya wavuvi kunyamaza wanapoona miili zaidi ikielea baharini.
“Polisi tunawajulisha, wanakuja, wanabeba maiti, lakini hakuna siku wametueleza ni za kina nani," alisema mvuvi mmoja wa Kunduchi aliyezungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina gazetini akihofia usalama wake.
"Wavuvi tunafahamiana na ikitokea mwenzetu amekufa au chombo kimezama majini tunafahamu.
"Lakini tangu Agosti mwanzoni tunaokota miili ikiwa imeandaliwa (imefungwa) kabisa na siyo ya wenzetu.”
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu jana kuwa miili iliyookotwa ni mitatu na haikuwa kwenye viroba.
“Hadi sasa taarifa za miili mingi kama hiyo kuokotwa nazisikia kwako," alisema Kamanda Mkondya. "Hao watu watueleze nasi tutachukua hatua, hatuna taarifa za miili iliyofungwa kwenye viroba au sandarusi.
"Miili mitatu iliyookotwa Kunduchi iko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na haijatambuliwa, wananchi wafike kuitambua.”
Lakini wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti kwenye maeneo ya uvuvi hayo jana, wavuvi walisema wamepokea taarifa kutoka wenzao wa eneo la Kizimkazi, Zanzibar, kwamba huko nako pia zimeokotwa maiti tano.
Mvuvi mmoja wa Kunduchi alisema siku mbili zilizopita ziliokotwa maiti tano katika eneo la Bongoyo na nne nyuma ya kisiwa cha Mbudya, jijini Dar es Salaam.
Alisema kati ya maiti tisa hizo, moja ilikuwa ya mwanamke na kwamba zilikuwa zimefungwa kamba miguuni, kichwani na tumboni.
"Zote zilikuwa zimeharibika na sura hazitambuliki," alisema na kueleza kuwa zilichukuliwa na polisi baada ya kutaarifiwa.
Alisema polisi waliochukua miili hiyo ni wa mkoa wa Kinondoni kutoka vituo vya Kawe ambayo ni wilaya ya kipolisi na Wazo Hill.
"Hawajawahi kusema mtu huyo alifia wapi na chanzo cha kifo, (hivyo) wengi tuna wasiwasi tu," alisema mvuvi mwingine ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe.
“Ukiangalia umri ni miaka 25 hadi 50.
"Jamaa zetu wa Feli waliokota maiti sita wiki mbili zilizopita (na) kati yake mbili zimefungwa pamoja na katika hizo moja ni mwanamke.
"Tulichozoea wavuvi ni kuokota maiti za wavuvi wenzetu ambaye alizama au kupotea, na zinakuwa na nguo zake za kawaida, lakini hizi ni za kuandaliwa.”
KICHWA CHINI
Kwa mujibu wa wavuvi hao, wanakutana na maiti nyingi zikiwa ndani ya viroba, ambapo marehemu wanakuwa waliingizwa humo kwa kutanguliza kichwa.
"Yaani mtu kaingizwa kichwa kichwa, akafungwa kwenye miguu, tumboni na shingoni,” alisema mvuvi huyo na kueleza zaidi:
“Nyingine utazikuta zipo tatu zimefuatana na nyingine mbili ndani ya kiroba kimoja.
"Na kuna wakati zimepangana nyingi kwa pamoja na kila kiroba na maiti yake.”
Mvuvi huyo alisema wanaogopa kuziopoa kwa sasa na kwamba nyingi ni za wanaume.
Chanzo hicho kilieleza kuwa maiti nyingi zinakutwa nyuma ya kisiwa cha Mbudya, kwenye mkondo mkuu (bahari kuu).
Alisema baadhi ya wavuvi walizifungua maiti hizo na kukuta zimeharibika vibaya.
"Walishindwa kula kutwa nzima," alisema na kueleza kuwa baadhi ya maiti zina majeraha ya kukatwa miguuni.
“Maiti tunazoona na kutoa taarifa ni zile zinazokuja kwenye maeneo yetu, lakini tunapokwenda kuvua eneo la bahari kuu huko tunazikuta nyingi na tunashindwa kutoa taarifa,” alisema.
“Kipindi hiki ni Kusi, kawaida yake asubuhi unavuma umande, ukifika saa sita au saba kama sasa hivi unavuma matalahi yanaingiza ndani kutoka bahari kuu kuleta huku (Kunduchi)."
Kwa mujibu wa wavuvi hao, maiti hizo zinatoka maeneo ya ama Dar es Salaam, Pwani, Lindi au Mtwara.
Walipoulizwa wamejuaje kama maiti hizo zinatokea maeneo hayo, wavuvi hao walisema bahari ina pepo kuu mbili ambazo ni za Kaskazini na Kusini na kwamba kila mmoja unavyopiga ndivyo vitu au maiti inaweza kusafiri na kukutwa katika eneo fulani.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, upepo wa sasa hivi unavuma kutoka kusini kwenda kaskazini, hivyo maiti hizo zisingeweza kuwa zinatokea Tanga ama Kenya, kwa mfano.
“Hakuna kinachotoka kaskazini kuja kusini, ukiona kimekuja huko kimevushwa na upepo kutoka kusini kuja huku,” alisema mmoja wa wavuvi.
Aidha, alisema kwa kawaida kama ni maiti ambayo haijaandaliwa huokotwa moja au mbili na ikiwa kwenye mavazi ya kawaida kama suruali au kaptula, lakini zinazookotwa kwa sasa zipo ndani ya viroba.
“Tuna shaka kubwa sana na hii miili, hatuna shaka kuwa siyo wavuvi wenzetu, tuna mtandao mkubwa kutoka Mtwara hadi Tanga tunafahamiana na tunahabarishana.
"Hata maiti ikiokotwa eneo jingine tunajua, lakini hizi hatujui kwa kuwa tumewasiliana na wenzetu hakuna vifo vingi vya wavuvi.”
Nipashe iliwatafuta viongozi wa serikali ya mitaa kwenye maeneo husika, ambao walisema wamelisikia suala hilo kutoka kwa wavuvi, lakini waulizwe polisi.

No comments:

Post a Comment