Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekosoa kitendo cha CCM kuweka mgombea wake kwenye nafasi ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki wakati haikutakiwa kufanywa hivyo, na kusema kwamba kitendo hicho kitasababisha mgogoro wa kidiplomasia.
Kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kutoka kwa chama hiko, imesema CCM imekiuka utaratibu wa Bunge hilo la kumtafuta Spika la kuliongoza kwa kumuweka mtu wao kwenye kinyang'anyiro, wakati kiutaratibu ilitakiwa Spika wa awamu hii atoke nchi ya Rwanda kulingana na mzunguko ambao ulikuwa unafuatwa, na kwamba kitendo hicho kinaweza kuleta migogoro itakayoathiri Jumuiya hiyo kama kipindi cha Idi Amin.
"Awamu hii Spika alipaswa kutoka Rwanda, lakini Tanzania kwa kuwa CCM imezoea kutokuheshimu sheria na kanuni zilizopo imemteua mbunge wake Adam Kimbisa kugombea nafasi ya Spika kinyume kabisa na kanuni za Bunge hilo, na huu ukiwa ni mwendelezo wa utamaduni wao wa kutokuheshimu sheria na kanuni, kitendo ambacho kinatishia ustawi na uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki", imeandika Taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa .."CHADEMA tunalaani kitendo hiki, CCM wajue kuwa watabeba lawama zote kama kutakuwa na mgogoro ndani ya Bunge la Afrika Mashariki ambayo unaweza kupelekea mgogoro wa kidiplomasia katika Jumuiya nzima kutokana na tabia yao ya kutoheshimu taratibu zilizowekwa. Ttunataka kanuni za EAC ziheshimiwe, kwani tunakumbuka matendo ya Idd Amin mwaka 1977 yalivyovunja Jumuiya hii, hatutaki yajirudie kamwe".
No comments:
Post a Comment